KUKOSANA, kupishana maneno, kutokuelewana na hata kugombana ni mambo ya kawaida katika uhusiano.
Ni mambo ambayo hayakwepeki, kwani hakuna watu wawili wanaofanana, kitabia ama kimwenendo.
Aina za ugomvi huwa zimetofautiana na suluhu yake pia itapatikana kwa jinsi ambavyo kukosana huko kulitokea. Upo ugomvi ambao ni wa kawaida na huisha kirahisi, kwamba mtazungumza wawili na kufikia muafaka bila kumshirikisha mtu ama watu wengine. Lakini pia kuna ugomvi ambao huwa patashika na mara nyingi wahusika huenda wasijue hatua ya kuchukua ili kuweka mambo sawa na hatimaye kusababisha ufa mkubwa baina yao.
Inapotokea kwamba umevurugana na mwenzako, mmekosa kuelewana na kuingia katika ugomvi, mmetoleana maneno yasiyofaa na wakati mwingine kudhalilishana, ni muhimu kwanza kutafakari chanzo hasa cha tofauti yenu.
Hatua hii ni ya muhimu sana, kwani iwapo nyote wawili mtashindwa kutambua kiini cha mgogoro wenu, itakuwa pia vigumu kuweza kuutatua. Mnaposhindwa kugundua chanzo cha tatizo, ndipo mnapokuwa chanzo cha tatizo.
Mara nyingi ugomvi huanza kwa vitu ambavyo huenda vikaonekana ni vidogo, ambavyo hatimaye huwa vikubwa na kusababisha mvutano zaidi.
Idadi kubwa ya wapendanao hukosana na ugomvi kuwa mkubwa kwa sababu ya vyanzo vidogo ambavyo walishindwa kuvigundua mapema na vikazaa matatizo mengine. Mfano rahisi, chanzo kinaweza kuwa mpenzi wako amekupigia simu lakini ukashindwa kuipokea kwa muda muafaka. Atakapopiga kwa mara nyingine au mkikutana, usitegemee atakufurahia kwa sababu atahisi umemdharau kwa kutopokea simu yake.
Endapo utafanya makosa ya kushindwa kuliona kosa lako mapema na kushindwa kuomba radhi au kutoa maelezo yanayoeleweka kwa nini hukupokea simu, matokeo yake utamjibu vibaya, naye atakujibu vibaya na mwisho mtaishia kupigana au kuachana kabisa mkiwa mmeshatoka kabisa kwenye kosa la msingi.
Bila shaka msomaji wangu umeona jinsi chanzo kidogo kinavyoweza kusababisha tatizo kuwa kubwa. Ndoa nyingi au uhusiano unaofika mwisho huwa umesababishwa na mambo madogo ambayo yalishindwa kutafutiwa suluhu mapema.
Katika kila ugomvi unaotokea, jambo la kwanza jipe muda wa kutafakari chanzo kilichosababisha mkagombana. Wakati mwingine wewe ndiye unaweza kuwa chanzo cha tatizo lakini kama ukiyajua makosa yako mapema na kukiri kisha kuomba radhi kwa mwenzio, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kurudisha mapenzi kwa haraka.
Pili, mpe muda mwenzako ili hasira zake ziishe. Kila binadamu ameumbwa akiwa na jinsi yake ya kushughulikia hasira zake na ni wachache wanaweza kuzidhibiti hasira. Ni rahisi mtu kutukana, kupiga au kuharibu vitu akiwa na hasira.
Inapotokea mnakosana, kila mmoja atakuwa na hasira zake na ili kuweza kuepusha mlipuko wa ugomvi ni vyema mkajipatia muda kwanza ili hasira zipungue.
Halikadhalika, mpe nafasi mwenzako atoe yaliyo moyoni mwake. Ni vigumu kumuelewa mtu kabla hujampa nafasi ya kuzungumza na kumaliza kile alichokusudia kukisema. Endapo tatizo limetokea na upo kwenye hatua za kusaka suluhu, mpe mwenzako nafasi ya kueleza dukuduku lililopo ndani ya moyo wake.
Usimkatishe wala kumbishia, muache aongee kilichomuudhi mpaka dukuduku lake liishe kisha na wewe jieleze kwa utulivu. Ni jambo la busara zaidi kuomba msamaha, hata kama unaona mwenzako ndiye aliyekosea. Hakuna silaha nzuri inayoweza kukusaidia kuushinda ugomvi wowote na kutulizz
Hata kama unaona dhahiri kwamba kosa sio lako, omba msamaha kwanza kisha baada ya hapo mueleweshe mwenzako hali halisi ya mambo. Kumbuka kwamba siku zote hasira ni hasara."
إرسال تعليق