KARIBUNI wapenzi wasomaji wangu katika safu hii ya mambo ya mahusiano inayowajia kila Jumanne na Jumamosi, ikilenga kujuzana hili au lile kuhusiana na suala zima la mapenzi.
Awali ya yote, nianze kutoa shukrani zangu za dhati kwa wote ambao wamekuwa wakichangia mada zangu, wakiwamo wale wanaouliza maswali ambayo hata hivyo ni vigumu kumjibu mmoja mmoja.
Baada ya salamu hizo, nigeukie mada ya leo ambayo inatokana na baadhi ya maswali ya wasomaji wangu ambao wamekuwa wakitaka kufundishwa jinsi ya kutongoza wasichana.
Kuna msomaji mmoja (jina kapuni) alisema kuwa amekuwa katika urafiki na msichana mmoja anayempenda sana lakini akishindwa kuwasilisha hisia zake na mwisho wa siku kujikuta akiumia moyoni.
Ndugu msomaji, kutongoza ni kitendo cha kumshawishi mtu kwa njia yoyote ili kukubaliana na matakwa yako.
Katika suala zima la mapenzi, kutongoza umekuwa ni mtihani mzito kwa baadhi ya wanaume kwani unaweza kumkuta mtu akiwa anampenda msichana fulani, lakini akitumia muda mrefu kufikiria jinsi ya kumnasa.
Wapo ambao wamekuwa wakitumia fedha ama kuwanunulia vitu vya thamani kama njia za kuwapata wasichana. Katika hilo, wapo wanaofanikiwa huku wengine wakiishia ‘kula za pua’.
Njia hiyo ya kutumia fedha au mali, inaweza kuzaa matunda kwa wasichana malimbukeni na washamba wa fedha au kitu husika. Lakini pia inaweza kuwa njia sahihi kwa wasichana ‘wadanganyaji’.
Lakini pia, wapo wale wanaowaeleza moja kwa moja wasichana kuwa wanawapenda na mwisho wa siku kufanikiwa kuwa nao ndani ya muda mfupi.
Ndugu msomaji, kwa msichana mwenye msimamo, anayejielewa na anayejiheshimu, kamwe huwezi kumpata kwa njia hizo hapo juu.
Wavulana au wanaume wengi wamejikuta wakigonga mwamba kwa wasichana wa aina hiyo na mwisho wa siku kujikuta wakiishia kuwakashifu kwa kila namna kisa tu wamekataliwa.
Kwa faida ya wale waliotaka kufahamu jinsi ya kuwatongoza wasichana, wafahamu kuwa kutongoza ni sanaa inayohitaji ubunifu wa hali ya juu.
Ni kama ilivyo katika sanaa ya uigizaji ambapo unaweza kumkuta mtu akiwa na kipaji cha hali ya juu kama alivyokuwa marehemu Steven Kanumba au Masoud Kipanya katika uchoraji katuni.
Hata katika kutongoza kuna ambao ni mafundi mno kiasi kwamba anapomtaka msichana, ni vigumu ‘kuchomoka’.
Ndugu msomaji, kutongoza hakuhitaji kiwango cha juu cha elimu, kuwa na fedha au mali nyingi, utanashati, cheo na mengine kama hayo.
Kuna njia ambazo zinaweza kumsaidia mwanamume kumnasa kirahisi mwanamke, hata awe mrembo kama Mmarekani Halle Berry anayetajwa kuwa mwanadada mweusi mkali kuliko wote duniani, akiwa ni mwigizaji na mwanamitindo aliyetwaa tuzo kibao.
Miongoni mwa njia hizo, kwanza ni kufahamu udhaifu wa msichana husika kuona ni vipi unaweza kutembelea udhaifu huo kumnasa.
Katika hilo, mathalani iwapo msichana unayemtaka anapendelea sana kuogelea, unaweza kuhakikisha hukosi maeneo anayopenda kwenda kuogelea na ikiwezekana kujumuika naye ili kukufanya kuwa naye karibu zaidi.
Kwa kufanya hivyo, unaweza kumfanya kukuona kama mtu wa karibu yake zaidi ambaye mnaendana (type yake) hali itakayomfanya kukuamini na kukuhitaji pale atakapokuwa akihitaji kampani.
Nakumbuka miaka ya 1995 hadi 1998, kuna rafiki yangu ambaye aliwahi kumpata msichana mrembo aliyekuwa akiwasumbua mno wavulana maeneo ya Keko, Dar es Salaam, baada ya kufanikiwa kufahamu ‘ugonjwa’ wake.
Msichana huyo, alikuwa akipenda kwenda kwenye maeneo yanayotolewa huduma za intaneti (Internet Café) hivyo kila alipomwona akitoka kwao, alikuwa akimfuata kwa nyuma hadi alipoelekea na kukutana naye huko.
Yule msichana baadaye alibaini kuwa yule jamaa ni jirani yake hivyo kila alipofikiria kwenda internet café, alimpitia ambapo utaratibu huo uliendelea na mwisho wa siku wawili hao kujikuta wakiwa wapenzi.
Hata hivyo, kuongozana na mtu pekee hakutoshi kumfanya kuwa mpenzi wako. Kinachotakiwa ni kuhakikisha unamteka kwa kujishusha na kuwa kama mtumwa wake, huku ukihakikisha unaziteka hisia zake kwa kauli na matendo.
Kwa upande wa matendo, unaweza kuhakikisha unapokuwa naye usiuogope mwili wake, kwa aidha kumshika mikono au hata kuziweka nywele au mavazi yake sawa pale ilipobidi kufanya hivyo kuonyesha jinsi unavyomjali, lakini pia kuonyesha ujasiri wako dhidi yake.
Kwa kufanya hivyo, utakuwa umemwathiri kisaikolojia na kujiweka karibu yake zaidi kiasi kwamba unapotupa ndoano, lazima itanasa.
Kwa leo hebu tuishie hapa, tukutane Jumanne ambapo tutaendelea na mada hii kwa faida ya wale walioomba kusaidiwa katika hilo.
Post a Comment